Wednesday, December 30, 2015

FANYA MAHUSIANO YAKO YAWE MAPYA.

Mwaka unakaribia kwisha umejifunza nini? Je, kupitia safu hii matatizo yameondoka , yamepungua au yameongezeka?
Kwa vile tunakaribia kuuanza mwaka mpya, basi napenda  tufanye utafiti kuhusiana na mwenendo mzima wa maisha yetu ya kimapenzi. Huu ndiyo muda muafaka wa kujichambua mwenyewe ulibeba vipi uhusiano ndani ya penzi lako.

Katika muda wote kulikuwa na migongano, je, chanzo chake nini? Kama ni wewe ni muda wako wa kujirekebisha ili usiwe chanzo cha matatizo ya kila siku.
Ni makosa mtu kurudia kosa moja kila mara, mwanadamu anayejitambua hujifunza kupitia lile linalokemewa sana na mwenzake, japokuwa unapenda kulifanya.

Sifa kubwa ya mwanadamu ni kufikiri kabla ya kutenda, siku zote mapenzi ni kusikilizana, kufarijiana na kubembelezana. Bila shaka mwaka uliopita kuna mambo yalitokea hadi kufikia hatua ya kutishia kuvunja ndoa au uhusiano wenu.
Mwaka umeisha, umekaa na kujiuliza tatizo nini? Umejichunguza na kujua labda wewe ndiye chanzo?
Mmeukaribia mwaka mpya, mmekaa kama wanandoa au wapenzi kumaliza tofauti zenu ili kuuanza mwaka nanyi mkiwa wapya?
Kama hamjakaa kujadili mwenendo mzima wa uhusiano wenu kwa mwaka mzima hamjachelewa. Hebu kupitia safu hii kaeni chini na kuchambua matatizo yote yaliyowakwaza sana.
Tafuteni sehemu tulivu ili kupata nafasi ya kuzungumza kwa kujiamini. Sehemu hii haitakiwi mmoja kujiona yupo juu ya mwenzake au ubishi kwa kile ambacho kimemgusa.

Mazungumzo yenu yawe ya kirafiki, kosoaneni kwa sauti za kawaida, ondoeni jazba kwani muda huo haina nafasi. Uwe mwepesi kukubali kosa na kuomba msamaha. Kwa vile nia yenu ni kujenga, hakikisheni yote yaliowakwaza mwaka huu unaoisha hamyapi tena nafasi.
Jiepusheni kuwa chanzo cha maumivu ya wenzenu, umeamua huyo awe wako wa kufa na kuzikana kwa nini muumizane? Sawa, mwanadamu ana upungufu, basi makosa yako yasiwe mazoea kwa vile tu upo juu ya mwenzako. 

Mapenzi hayaangalii cheo, fedha wala uzuri wa sura na umbile, bali kujitoa kwa ajili ya mwenzako.
Jutia makosa uliyofanya mwaka huu unaoishia na kutokuwa tayari kuyarudia, hii itakufanya mwaka ujao uwe makini sana na kumfanya mpenzi wako asahau maumivu ya mwaka huu. Muahidi mpenzi wako kuwa mwaka unaoanza utakuwa sehemu ya furaha yake ya kila siku, kama utakwenda tofauti basi utakuwa msaliti.
Kiapo hiki si cha mtu mmoja bali kiwe cha wote. Kama kweli unayoyasema yanatoka moyoni na kuwa tayari kutorudia yaliyomkwaza mwenzako mwaka huu, basi mwaka ujao utakuwa wa furaha na amani. Nakutakieni maandalizi mema ya kuukaribisha mwaka mpya wenye mapenzi ya dhati, kila mmoja awe sehemu ya furaha ya mwenzake.